Monday, 9 November 2015

VURUGU ZAENDELEA KULINDIMA BURUNDI

 
Amri ya kuwapokonya silaha wapinzani iliyotolewa na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, imesababisha watu kadhaa kuuawa nchini humo. Kwa mujibu wa duru za habari hadi sasa jumla ya watu tisa wameuawa siku na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa hivi karibuni na watu wenye silaha nchini humo.
Kabla ya hapo Rais Pierre Nkurunziza, alikuwa ametoa muhula wa kufikia Jumamosi usiku kwa wapinzani kuhakikisha wanasalimisha silaha zao kwa jeshi la nchi hiyo na kwamba, wangepata msamaha. Kwa mujibu wa amri ya Rais Nkurunziza, baada ya muda huo jeshi litalazimika kutumia nguvu kwa ajili ya kuwavua silaha waasi iwapo hawatakuwa tayari kutii amri hiyo. Mashuhuda wanaeleza kuwa, watu waliokuwa wamevalia sare za polisi jana usiku waliwamiminia risasi wateja waliokuwa nje ya mgahawa mmoja ambao mara nyingi hukusanyika wapinzani wa serikali, kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura. Punde baadaye, mamia ya askari polisi walianzisha msako mkali wa kuwapokonya silaha waasi katika maeneo ya kaskazini mwa mji huo. Hii ni katika hali ambayo Rais Paul Kagame wa Rwanda ameelezea wasiwasi wake juu ya kukaririwa mauaji ya kimbari ya nchi yake huko Burundi. Rais Kagame amewataka viongozi wa serikali ya Bujumbura kuzuia ghasia zinazofanana na zile za Rwanda ambazo ziliitumbukiza nchi hiyo kwenye mauaji ya kizazi mnamo mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment