Monday, 9 November 2015

MAGUFULI ASIMAMISHA BODI YA HUDUMA HOSPITALI YA MUHIMBILI

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amesimamisha bodi ya afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia huduma mbovu hospitalini hapo.
Rais Magufuli amechukua hatua hiyo wakati alipofanya safari ya kushtukiza katika hospitali hiyo ya taifa na kutembelea wodi za Mwaisela, Sewa Haji na idara nyingine muhimu, ambapo alikasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi hususan mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile, MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa. Katika ziara hiyo ya ghafla hospitalini hapo, Rais Magufuli alipata kutembelea maeneo muhimu huku akikutana na wagonjwa ambao baadhi yao walikuwa wamelala chini kwa kukosa vitanda na kuongea nao kwa karibu. Aidha aliongea na wauguzi ambapo pia alisikiliza kutoka kwao changamoto mbalimbali zinazowakabili. Watu mbalimbali walifurika katika kumpungua mkono Rais Magufuli huku wakionyesha matumaini makubwa ya kutekeleza ahadi alizozitoa katika kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani hivi karibuni. Awali Rais Magufuli alifika katika Hospitali ya Agha Khan kumjulia hali Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo Bisimba anayepatiwa matibabu na vipimo katika hospitali hiyo baada ya jana kupata ajali katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam, Tanzania.

No comments:

Post a Comment